Advertisement

Israel yatoa wito kwa Hamas kujisalimisha huku jeshi likishambulia mji wa Gaza

Israel imetoa wito tena kwa Hamas kujisalimisha huku jeshi likiendeleza mashambulizi katika jiji la Gaza ambako mamia kwa maelfu ya Wapalestina wanatafuta hifadhi.

Waziri wa mambo ya nje Gideon Saar aliwaambia waandishi wa habari mjini Jerusalem kuwa vita hivyo vinaweza kumalizika mara moja iwapo Hamas itawaachilia mateka waliosalia wanaoshikiliwa Gaza na kuweka chini silaha zake.

“Tutafurahi zaidi kufikia lengo hili kwa njia za kisiasa,” alisema.

Katika kujibu, afisa mkuu wa Hamas Basem Naim aliambia Reuters kwamba haitaweka silaha zake chini lakini itawaachilia mateka wote ikiwa Israeli itakubali kumaliza vita na kuondoa vikosi vyake kutoka Gaza, msimamo ambao kwa muda mrefu umekuwa wa kundi hilo la wapiganaji wa Palestina.

Israeli mwezi uliopita ilianzisha mashambulizi katika mji wa Gaza, na vikosi vyake sasa viko kilomita chache tu kutoka katikati mwa jiji.

Usiku kucha, mashambulizi yaliwauwa watu 14 kote jijini, maafisa wa afya wa eneo hilo walisema, ikiwa ni pamoja na shambulizi kwenye shule iliyo kusini mwa mji wa Gaza ambayo imewahifadhi Wapalestina waliokimbia makazi yao.